UPATANISHI KATIKA SENTENSI YA KICHUKA, KENYA

By :  Julius Gitonga

Year : 2014

Level : Masters 

IKISIRI
Utafiti huu ulichunguza upatanishi katika sentensi ya lahaja ya Kichuka. Lahaja ya Kichuka huzungumzwa katika tarafa za Chuka na Mariani katika kaunti ndogo ya Meru Kusini katika kaunti ya Tharaka Nithi. Mwauo wa maandishi ulibainisha kuwa hakuna utafiti uliofanywa kuhusiana na suala la upatanishi katika Kichuka. Kwa hivyo, utafiti huu ulikusudia kuchunguza upatanishi katika lahaja ya Kichuka ili kulijaza pengo hili. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Utawala na Ufungami iliyoasisiwa na Chomsky 1981. Nadharia hii ilifaa utafiti huu kwa sababu huchunguza uhusiano baina ya viambajengo katika sentensi hasa uhusiano wa kiupatanishi kati ya virai nomino na virai vitenzi. Modula mbalimbali za nadharia hii: Eksi-baa, Funge, Uhusika, Utawala, Theta na Ufungami zilitumika. Kupitia modula hizi, viambishi vya upatanishi katika sentensi za Kichuka vilibainishwa na kufafanuliwa. Data ya utafiti ilikuwa sentensi za Kichuka ambazo mtafiti alizitunga mwenyewe kutokana na umilisi wake kama mzawalugha wa Kichuka. Utafiti vilevile ulifanywa maktabani ambamo habari muhimu kuhusu mada ya utafiti zilipatikana Kwa jumla, sentensi za Kichuka 200 zilizojumuisha; sentensi sahili, ambatani na changamani zilishughulikiwa. Katika awamu ya uchanganuzi, sentensi hizi zilipangwa kwa mujibu wa uwiano wa viambishi vya upatanishi katika kategoria za vivumishi na vitenzi. Majedwali, vielelezo vya ngoe na kanuni miundo ilitumiwa kutathmini ruwaza za upatanishi zilizodhihirika katika ngazi ya uchanganuzi. Maelezo yalitolewa kuhusiana na ruwaza hizo kwa kuzingatia ngeli za nomino zilizobeba majukumu ya k-amri katika sentensi husika.Imegunduliwa katika utafiti huu kuwa upatanishi kati ya virai nomino vya mtenda na virai vitenzi ni wa lazima katika Kichuka na kuwa si lazima kuwepo na upatanishi kati ya virai nomino vya mtendwa na virai vitenzi. Upatanishi unapotokea baina ya viambajengo hivi, lazima kirai nomino kinachorejelewa na kipatanishi kidondoke kwa sababu kategoria zote mbili haziwezi kutokea katika muundo mmoja katika sentensi ya Kichuka. Matokeo ya utafiti huu yanakusudiwa kuchangia isimu miundo na uelewa wa lugha za Kibantu na wanafunzi na walimu. Pia utasaidia lugha za Kibantu kufanyiwa utafiti zaidi pamoja na kufanikisha utafiti katika isimu linganishi. Aidha, utasaidia kuhifadhi lahaja ya Kichuka katika maandishi.

 

Chuka University :ISO 9001:2015 Certified.  Copyright © 2017  Chuka University. All Rights Reserved.