MWINGILIANOMATINI KATIKA TAMTHILIA YA KISWAHILI: MFANO WA MASHETANI NA KIJIBA CHA MOYO

By : Ambrose Ngesa Kang'e

Year : 2014

Level : Masters 

ABSTRACT

 

Tamthilia ya Kiswahili ni mojawapo ya tanzu za fasihi andishi ya Kiswahili. Tanzu nyingine za fasihi hii ni pamoja na riwaya, ushairi hadithi fupi na novela. Utanzu wa tamthilia ya Kiswahili umedhihirisha, kwa njia moja au nyingine, uhusiano wa kimatini.Wahakiki wameweza kuchunguza nyanja kadhaa za utanzu wa tamthilia kama vile: utunzi wa tamthilia, mwathiriano, usemezano, maendeleo ya maudhui, wahusika na mtindo. Utafiti huu ulilenga kuchunguza na kuchanganua mwingilianomatini katika tamthilia ya Kiswahili. Viwango na aina za mwingilianomatini zilichunguzwa na kubainishwa. Ulitumia mbinu ya kitahamano ya utafiti na kuongozwa na nadharia ya mwingilianomatini iliyoasisiwa na Julia Kristeva (1966). Utafiti huu ulifanyiwa maktabani na kuhusisha tamthilia mbili za Kiswahili: Mashetani (Hussein, 1971) na
Kijiba cha Moyo (Arege, 2009). Tamthilia hizi ziliteuliwa kimakusudi na kushirikishwa katika utafiti. Data iliwasilishwa na kuchanganuliwa kwa njia maelezo. Vifungu vilivyodhihirisha uhusiano wa kimatini vilidondolewa kutoka tamthilia zote mbili na kupangwa kuchanganuliwa. Imebainika kwamba kuna mwingilianomatini baina ya tamthilia ya Mashetani na Kijiba cha Moyo. Kadhalika, imebainika kwamba maudhui na fani zimechangia viwango vya mwingilianomatini katika tamthilia hizi mbili zilizochunguzwa. Vilevile, imebainika kuwepo kwa urejelezi, mwigo na wigobezi kama aina za mwingilianomatini baina ya matini za tamthilia hizi mbili. Matokeo ya utafiti huu yanachangia maandishi ya kitaaluma katika uhakiki wa fasihi linganishi. Vilevile, unatarajiwa kuwa mwongozo wa kuelewa nadharia ya mwingilianomatini kwa wahakiki, wahadhiri, walimu na wanafunzi wa somo la fasihi linganishi. Tasnifu hii ina sura tano. Sura ya Kwanza ni utangulizi wa utafiti ambapo mtafiti ameshughulikia usuli wa mada, misingi ya uteuzi wa mada, suala la utafiti madhumuni ya utafiti, umuhimu wa utafiti, upeo wa utafiti, pamoja na maelezo ya istilahi muhimu. Sura ya Pili imeshughulikia mwauo wa maandishi, dhana ya mwingilianomatini na kisha kuhitimishwa kwa kueleza misingi ya nadharia ya mwingilianomatini. Sura ya Tatu imetoa maelezo kuhusu mbinu za utafiti na uchanganuzi wa data. Sura ya Nne imeshughulikia uwasilishaji na uchanganuzi wa data. Sura ya Tano imehitimisha utafiti huu kwa kutoa muhtasari, kuonyesha matokeo, pamoja na kutoa mapendekezo ya utafiti zaidi.

Chuka University :ISO 9001:2015 Certified.  Copyright © 2017  Chuka University. All Rights Reserved.