UCHANGANUZI WA MCHONGOANO KATIKA TAIFA LEO KAMA SANAA YA VICHEKESHO VYA UREKEBISHAJI WA JAMII

JAMES MUCHANGI NDWIGA

IKISIRI

Vichekesho ni uwanja unaoingiliana na taaluma mbalimbali. Wataalamu wengi wamekuwa akishughulikia vichekesho katika nyanja za  saikolojia, falsafa, isimu-sosholojia na fasihi. Utafiti huu ulilenga  kuchunguza na kuchanganua mchongoano kama vichekesho vya urekebishaji wa jamii nchini Kenya.  Ulichunguza vipengee vya muundo, mtindo, maudhui na dhima, katika  mchongoano na  jinsi  vinavyoumana kimatini ili kujenga vichekesho  rekebishi.    Madhumuni yalikuwa kuchanganua ruwaza za kiisimu katika mchongoano kama vichekesho vya urekebishaji wa jamii na kufafanua ruwaza hizo.   Ulitumia mbinu ya kithamano ya utafiti na kuongozwa na nadharia ya  Vichekesho Rekebishi ya  Bergson (1980).    Utafiti huu ulifanyiwa maktabani na  ulizingatia vifungu 52 vya michongoano kutoka safu zote 52 za  Hekaheka  za  Wiki  na  Mikikimikiki  katika magazeti ya  Taifa Leo, kwa kipindi cha mwaka mmoja, wa 2011.    Vifungu hivi 52 viliteuliwa kimakusudi na  kushirikishwa katika utafiti.    Data iliwasilishwa  na kuchanganuliwa kwa njia ya maelezo.    Ruwaza  za kiisimu za kila kifungu zilitambuliwa.Utafiti ulibaini kuwa mchongoano una muundo na mtindo maalum pamoja na kuendeleza dhima ya urekebishaji kama sanaa ya vichekesho vya urekebishaji wa jamii.    Ilibainika kuwa kwa kutumia chuku, dhihaka na kejeli, mchongoano huwa na nafasi kubwa ya urekebishaji wa jamii ambao hupaniwa wakati wa kutungwa.    Matokeo ya utafiti huu yanachangia fani ya  vichekesho,  uchambuzi wa kidiskosi, isimujamii, semantiki na pragmatiki.  Vilevile unafaidi wahakiki wa fasihi na lugha kama ala ya utambulisho. Sura ya Kwanza ilishughulikia usuli wa mada, suala la utafiti,  madhumuni, misingi ya uteuzi na upeo wa  utafiti.    Sura ya Pili ni mwauo wa maandishi na Sura ya  Tatu kushughulikia mbinu za utafiti na uchanganuzi wa data.    Sura ya Nne ilihusu uwasilishaji na uchanganuzi wa data kisha    Sura ya Tano kuhitimisha kwa muhtasari, matokeo na mapendekezo.

 

 

 

 

 

Chuka University :ISO 9001:2015 Certified.  Copyright © 2017  Chuka University. All Rights Reserved.