USAWIRI WA MWANAMKE NA WATUNZI WA TAMTHILIA NCHINI KENYA: MFANO WA TAMTHILIA ZA UASI, MAMA EE NA CHAMCHELA 

JOHN KIMATHI NKANATHA

2013

IKISIRI

Jamii nyingi za Kiafrika ni za kuumeni na  humweka mwanamke katika ngazi ya chini  akilinganishwa na mwanamume. Ili kuinua hadhi za wanawake, mashirika ya  kitaifa na ya  kimataifa yameweka mikakati  ya  kuboresha hadhi ya wanawake.  Fasihi ni  mojawapo ya vigezo ambavyo  jamii  inaweza kutumia kuendeleza na kudumisha  utamaduni  wake. Kwa vile fasihi ni amali ya jamii, inabadilika    kadiri jamii inavyobadilika.  Utafiti huu linganishi umetathmini mchango wa  waandishi  wa fasihi ya Kiswahili katika  kusawiri jinsi  jamii inavyomchukulia mwanamke. Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuchunguza jinsi waandishi wa tamthilia ya Kiswahili wanavyochangia  juhudi za kubadilisha mielekeo ya jamii  kupitia kwa fasihi ambayo  ni wenzo muhimu katika kuleta mabadiliko katika jamii.  Kwa hivyo, fasihi inaweza kutumiwa kubainisha jinsi jamii na utamaduni unavyobadilika. Kwa kuzingatia haya, utafiti huu ulilenga kubainisha mchango wa waandishi wa tamthilia katika kutetea haki za wanawake.  Huu ulikuwa utafiti wa maktabani ambapo tamthilia zilizochaguliwa na matini zinazohusu Ufeministi wa Kiafrika zilisomwa na kuchambuliwa.  Utafiti ulitumia sampuli makusudi  kulinganisha jinsi waandishi wa tamthilia; yaani Jay Kitsao - Uasi, Ari Katini Mwachofi - Mama Ee na Timothy Arege  -  Chamchela,  wanavyowasawiri wanawake katika jamii. Kwa vile kazi hizi  ziliandikwa  katika vipindi  tofauti  (Kitsao, 1980; Mwachofi, 1987;  Arege,  2007) tuliweza kubaini  jinsi  fasihi kama kipengele cha utamaduni inavyobadilika.  Utafiti uliongozwa na  Nadharia ya Ufeministi wa Kiafrika katika  kutathmini  jinsi  waandishi  wa tamthilia wanavyomsawiri mwanamke Mwafrika katika fasihi na nafasi anayopewa katika jamii. Nadharia hii inahusu utetezi wa haki za mwanamke Mwafrika na inatambua kwamba amedhulumiwa na kunyimwa haki.  Data ilikusanywa kwa kuzisoma  na kuzichambua  tamthilia  zilizoteuliwa ili kubainisha na kulinganisha jinsi wahusika wa kike na wa kiume walivyojengwa na kusawiriwa.  Matokeo ya utafiti  ni  kwamba  kupitia kwa fasihi, waandishi wana nafasi na mchango katika kuleta usawa wa jinsia katika jamii pana.  Utafiti utasaidia mashirika yanayohusika na  utetezi wa haki za    wanawake  na kuhimiza matumizi ya fasihi kama njia mojawapo ya kuelimisha watu na kuwahamasisha kuhusu maswala nyeti ya kijamii.

 

 

 

Copyright © 2019  Chuka University. All Rights Reserved.